MAKALA: Jinsi ya kujipanga 2016 kwa mafanikio endelevu


Bila shaka wasomaji wangu bado mnaendelea kusherekea Mwaka Mpya wa 2016 baada ya kuvuka 2015. Ni vizuri kujipongeza na kutafakari ulifanya nini mwaka jana.

Ni vyema ukafahamu kuwa ulikuwa wa mafanikio au wa hasara? Je, mipango yako uliyojiwekea umefanikiwa ?, bila shaka majibu ya maswali hayo ndiyo yatakayotoa dira yako ya mwaka huu wa 2016.

Kama ulifanikiwa una kila sababu ya kujiimarisha ili mambo yaendelea kuwa hivyo 2016. Kama hukufanikiwa ni wakati wa kuweka mikakati ya mafanikio. Lazima kila mtu kuhakikisha unapiga hatua mbele ya maendeleo.

Kuwa na mpangilio wa utekelezaji. Jambo lisilokuwa na mpangilio unaoeleweka, mtiririko mzima husababisha jambo kuchukua muda mwingi kufanikishwa. Hivyo kuchelewa kimaendeleo.
Maendeleo ninayozungumzia hapa ni yale ya kiuchumi kwa ajili ya wakati huu na ya muda mrefu ujao. Ni wazi tunakabiliwa na majukumu mengi kuanzia ya binafsi, familia na jamii inayotuzunguka. Yote hayo ni mambo ambayo mtu anapaswa kuyatatua kwa hali na mali. Niliwahi kuandika makala juu ya hali halisi kwamba kutofikiri leo umempa mtu nafasi akufikirie na kisha kukutawala pasipo wewe kufahamu. Ndugu yangu, binadamu wote ni sawa, ila tunafanyaje ili kuutimiza huu usawa?
Wachunguzi wa mambo wanasema asilimia tatu ya watu duniani wana malengo. Wameweka mikakati ya namna ya kuwa na mafanikio tena kwa kuyaandika ama kuyaorodhesha na kupanga nini kianze na kipi kimalizikie.

Asilimia 97 ya watu duniani hawana malengo maishani mwao. Kwa lolote tu lile likitokea basi, na wao humohumo. Kwa kifupi ni kusema mafanikio kwao yanapatikana kwa kubahatisha tu.
Hii inatokana na kukosa muda wa kufikri ili wajikomboe. Kuna mambo niliwahi kujifunza kwa wanazuoni mbalimbali, mmojawapo ni Dk John Maxwell katika kitabu chake cha “Thinking for Change”. Kuna jinsi mbalimbali za kufikiri ambazo zina tija kama ukiwa makini.

Moja ni kufikiri kwa zingatio jambo moja. Ina maana ondoa mambo mengine yote, fikiria ama tafakari jambo moja. Uwezo wa kufikiri kwa kuondoa mambo yanayochanganya kwenye akili yako, kutakusaidia kulinyambua jambo husika kwa kina.

Hatua ya pili ni kufikiri kwa ubunifu. Jambo la tatu ni kufikiri kimkakati. Panga ratiba au mkakati wa utekelezaji wa mipango yako. Jambo unalopaswa kuzingatia pia ni kuzingatia suala la muda. Tumia muda vizuri. Muda ni hazina ambayo ikipotea hairudi tena na pia lazima mtu anayepoteza muda siku atakuja kuulipia kwa namna yeyote ile.

Wanadamu wote tuna saa 24, je, umeshawahi kujiuliza katika muda huo umeutumia vipi kutengeneza vitu vipya au kuongeza thamani katika maisha yako?
Ukiona una majukumu mengi kiasi kwamba huwezi kutekeleza yote katika saa 24 ili kuharakisha maendeleo jipange kuajiri watu wa kukusaidia kufanikisha hayo. Mtu aliyewekeza huajiri watu ili wafanikishe lengo la faida aliyokusudia.

Je, wewe muda wako wa saa 24 una kutosha? Kama siyo je huo muda ambao haukutoshi unautumia kwa ajili yako zaidi au unautoa bure kuangalia runinga, tamthilia, kupiga simu zisizo na masilahi, kuingia na kukaa mitandao ya kijamii siku nzima?

Kama haupo makini katika kutumia muda wako jua una deni kwa sababu ya kuja na kuishi hapa duniani. Kuna sababu ambazo husababisha watu wengi kushindwa kuutawala muda vyema.
Kutokuwa na malengo. Ni ngumu kufanikisha jambo kama hujaweka malengo ambayo yanaeleweka mfano nini unataka, lini, wapi, kiasi gani na kadhalika.

Jifunze pia namna ya kupata mafanikio. Hapa unapaswa kujifunza kuwa bingwa wa kutumia muda na siyo kusema; ‘muda si rafiki.’ Weka kumbukumbu ya mambo yako na uwe na muda wa kutathmini juu ya yale uliyoyafanya. Tafuta muda wa utulivu ili utafakari juu ya mipango yako.

Mtu anayetafakari mambo ana faida kubwa nyingi. Mojawapo ni kuepuka kutumia muda mwingi wa ufanyaji jambo fulani kwa kuwa hutumia kanuni. Katika hali hiyo huwa na uwezo wa kujiamini vya kutosha kwa sababu ni jambo la msingi ambalo limejengwa kwa kutokurupuka.
Wiki ijayo nitaelezea maeneo ambayo mtu akiwekeza mwaka huu ana nafasi kubwa ya kupata mafanikio.

Na; Deogratius Kilawe,Mkurugenzi wa Excel.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »