MWAKA 2009, Tanzania iliweka rekodi ya kuvutia baada ya kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).
Michuano hiyo mipya iliyofanyika wakati huo mara ya kwanza nchini Ivory Coast, lengo lake ni kuwapa nafasi wachezaji wa Afrika wanaocheza ligi za ndani kuwa na mashindano yao makubwa yenye hadhi.
Pengine kwa kutambua kwamba mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) hutawaliwa na mastaa wengi wanaocheza nje ya Afrika hasa Ulaya, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likaja na wazo la kuanzisha CHAN.
Hata hivyo tangu wakati huo, Tanzania haijapata tena nafasi ya kushiriki mashindano hayo licha ya kushiriki mara zote katika hatua za awali za kuwania kufuzu hali ambayo kimsingi haipendezi kwa taifa kubwa kama Tanzania.
Mashindano ya CHAN, bado machanga hasa kwa kuwa hayajafikisha hata miaka 10 hadi sasa na ni wazi kwamba kadri siku zinavyokwenda ndivyo yatakavyozidi kuwa makubwa
Mwaka huu, mashindano hayo yanafanyika nchini Rwanda na mbali na Tanzania kushindwa kufuzu, bado kuna eneo lingine ambalo Tanzania imetupwa katika mashindano hayo.
Pamoja na uchanga wa CHAN lakini Tanzania pia imetupwa kwenye waamuzi, katika orodha ya waamuzi iliyopatikana hivi karibuni wametajwa waamuzi zaidi ya 20 huku jina la mwamuzi wa Tanzania likikosekana.
Hili ni jambo ambalo limetugusa na ingawa hatutaki kuingia kwa undani kuhusu vigezo lakini jambo moja linalokuja katika fikra ya kila mdau wa soka ni swali la kwanini waamuzi wa Tanzania hawamo.
Akikosekana mwamuzi kwenye Kombe la Dunia au Afcon kidogo jambo hilo linaweza kuonekana la kawaida lakini katika CHAN, mashindano ambayo ni machanga wadau wa soka wana haki ya kujiuliza.
Ni kwa mtazamo huo huo tunapenda kuwakumbusha waamuzi nchini wajiulize nini hasa tatizo, ni kwanini waamuzi wa Tanzania hawamo kwenye CHAN.
Waamuzi watafakari jambo hili kwa mapana ili wajue nini hasa kilichowakwaza kiasi cha kukosa nafasi ya kuwamo kwenye CHAN hasa baada ya timu ya Tanzania kushindwa.
Mbali na maslahi ambayo mwamuzi anaweza kuyapata kwa kuwa katika mashindano haya lakini kama nchi ni heshima ya kipekee, kila Mtanzania bila kujali ni shabiki au si shabiki wa soka anafarijika kuona mwamuzi wa Tanzania akipeperusha bendera nje ya nchi.

EmoticonEmoticon